Siku 11 baada ya mbunge wa Mbeya, (Chadema) Joseph Mbilinyi maarufu ‘Sugu’ kuachiwa huru, kesho Mei 21, 2018 ataingia bungeni.
Sugu ataingia bungeni kuwawakilisha wananchi wa Mbeya baada ya kulikosa bunge hilo la bajeti tangu lilipoanza Aprili mwaka huu.
Sugu amesema: “Nipo Dodoma tayari, nimekuja baada ya hali ya mama yangu kuendelea kuimarika na kesho (Mei 21,2018) nitaanza kuwawakilisha wana Mbeya walionituma.”
“Wana Mbeya walikosa mwakilishi, walikosa wa kuwasemea mambo yao, kwani kilichotokea juu yangu ilikuwa kuwanyima fursa Mbeya kusikika ndani ya mjengo, sasa nimerudi kuwatumikia kwa nguvu zangu zote.”
Amesema kile kilichomtokea kimemwongezea umaarufu zaidi ya aliokuwa nao, “unajua mimi nilikuwa maarufu lakini kwa hiki kilichonitokea, nimekuwa mashuhuri na si maarufu tena.”
“Nikiwa njiani, Makambako wananchi wamenipa pole na wengine pongezi, sawa na Iringa na hapa Dodoma na kila mahali ninapopita, watu wanapiga picha na mimi, sasa utasema ni maarufu, mimi ni mashuhuri,” ameongeza:
Sugu na Katibu wa Chadema, Kanda ya Nyasa, Emmanuel Masonga walihukumiwa Februari 26, 2018 kwenda jela miezi mitano na Mahakama ya Hakimu Mkazi, Mbeya baada ya kuwakuta na hatia ya kutoa lugha ya fedheha dhidi ya Rais John Magufuli.
Mei 10, Sugu na Masonga waliachiwa huru kwa msamaha wa Rais Magufuli alioutoa Aprili 26, 2018 wakati wa sherehe za Muungano
No comments:
Post a Comment