Katibu Mtendaji wa Baraza la Sanaa la Taifa (Basata), Godfrey Mngereza amesema mwanamuziki Nassib Abdul maarufu Diamond amefanya makosa kumjibu Naibu Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Juliana Shonza akifananisha kitendo hicho na kuitukana Serikali.
Diamond Platnumz na naibu waziri huyo waliingia katika vita ya maneno baada ya Serikali kufungia nyimbo 15 mwezi uliopita, zikiwemo mbili za mwanamuziki huyo.
Mngereza amesema Diamond anapaswa kuelewa kwamba maneno machafu anayoyatoa dhidi ya waziri huyo ni sawa na kuitusi serikali jambo ambalo hata ukienda katika sheria za kimtandao anaweza kujikuta anaingia matatizoni.
Mngereza amesema wamesikitishwa na kauli ya Diamond na kusisitiza kwamba ni vyema akafuata taratibu katika kulalamikia suala hilo ikiwemo kuandika barua kama alivyomuelekeza Waziri Shonza.
Ameongeza kuwa si lazima msanii aandikiwe barua pale anapokosa kama ambavyo Diamond ameeleza katika ukurasa wake wa Twitter, kwamba Shonza angemwandikia barua kabla ya kumfungia.
Amebainisha kuwa si kila mwanamuziki anayefanya makosa huwa anaandikiwa barua.
Katika malalamiko yake, Diamond amesema naibu waziri huyo amekuwa akikurupuka kufungia nyimbo na pia kutowaandikia barua rasmi ndio maana ameamua kuyazungumza kwenye redio na mitandao ya kijamii.
Jana Waziri Shonza alisema hawezi kujibizana na Diamond kwa sababu alichofanya si maamuzi yake binafsi na kwamba kama anaona ameonewa apeleke malalamiko yake kwa maandishi.
No comments:
Post a Comment