Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Vincent Mashinji amehojiwa na polisi kuelezea namna anavyowafahamu watu waliofanya shambulio la risasi kwa Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu.
Akizungumza jana baada ya kutoka katika mahojiano hayo na maofisa wa polisi, Dk. Mashinji alisema maofisa hao walimtaka kuelezea alichowaambia waandishi wa habari katika mkutano wake nao mara baada ya kutokea kwa tukio hilo ambapo alionyesha dalili ya kuwafahamu waliohusika na tukio hilo.
“Niliwataka kurejea kwenye yale mazungumzo ili kuangalia kama nilionyesha dalili ya kuwafahamu watu hao au la.
“Baada ya kuwaambia hivyo walirejea kwenye mazungumzo hayo na kubaini kuwa katika kauli zangu sikuonyesha kama nilikuwa nawajua watu hao bali niliwataka wananchi kufufua polisi jamii ambayo itasaidia kuimarisha ulinzi,” amesema.
Dk. Mashinji amesema kutokana na hali hiyo, maofisa hao wa polisi walitaka kujua kama anazo taarifa zozote kuhusiana na tukio hilo ambapo alijibu hana taarifa hizo ila aliwataka polisi kuhakikisha waliofanya tukio hilo wanakamatwa na kufikishwa kwenye mikono ya sheria.
Mahojiano hayo ya polisi na Dk. Mashinji, yanatokana na wito wa Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma, Gilles Muroto ambaye alimtaka kiongozi huyo kufika kwenye Ofisi ya Polisi ya Mkoa wa Dodoma au Ofisi ya DCI kwa ajili ya mahojiano.
No comments:
Post a Comment